Lori lagonga magari saba, laua na kujeruhi Dar es Salaam

Wasamaria wema wakimwokoa Yahaya Makame mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam na mwenyeji wa Zanzibar kutoka katika gari lake dogo lilikandamizwa na lori la mafuta liloluwa likitoka Ubungo kuacha njia na kuyagonga takriban magari saba yalikuwa kwenye foleni kuelekea Ubungo upande wa pili wa barabara. Takriban watu watatu walifariki na wengine kujeruhiwa kwenye ajali hiyo. Picha ndogo ni Yahaya akiwa kwenye gari la polisi baada kuokolewa.

SIMANZI na majonzi jana vilitawala eneo la River Side, Dar es Salaam baada ya ajali mbaya iliyohusisha lori la mafuta na magari mengine madogo saba kusababisha vifo vya wawili papo hapo na wengine wanne kujeruhiwa vibaya. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema ajali hiyo ilitokea majira ya saa saba mchana na kwamba maiti na majeruhi wote walipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Ilala, Amana.

Lori la mafuta aina ya Marcedes Benz la Kampuni ya Dalbit lililokuwa likielekea Buguruni liliacha njia na kuyagonga magari saba yaliyokuwa kwenye foleni ya kuelekea Ubungo. Magari mengine yaliyohusika katika ajali hiyo ni Toyota Noah, BMW, Toyota Canter na Toyota Corolla nne. Mmoja wa waliofariki dunia ni mama mmoja ambaye mwili wake ulitenganishwa kabisa na kichwa baada ya gari alilokuwemo kukandamizwa na lori hilo.

Habari kutoka eneo la tukio, zilieleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni lori hilo kuacha njia, baada ya dereva wake kutaka kumkwepa mtembea kwa miguu ambaye alielezwa kuwa ni mama mjamzito. Watu hao wawili waliofariki dunia walikuwa kwenye magari tofauti.

Hata hivyo, habari nyingine zinadai kwamba miongoni mwa waliofariki katika ajali hiyo ni mchuuzi kanda za video ambaye alikuwa akitembeza biashara yake katika eneo hilo. Baadhi ya majeruhi walisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa lori hilo la mafuta baada ya dereva wake kushindwa kulimudu alipojaribu kumkwepa mtembea kwa miguu aliyekuwa anavuka barabara.

“Nilikuwa naelekea Ubungo nikiwa katika foleni, mara nikaona lori la mafuta likiwa linahama njia na kuja upande wetu. Baadaye kidogo, sikuelewa tena kilichokuwa kimetokea,” alisema Yahaya Makame.

Makame ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema licha ya kutokea kwa ajali hiyo mbaya, hakukuwa na msaada wowote wa haraka zaidi wa wakazi wa eneo hilo na wapita njia waliojitokeza kushuhudia. “Ajali imetokea saa 7:00 mchana, lakini, waokoaji wanafika saa 8:00.

Muda wote huo watu walikuwa bado wako ndani ya magari hayo wakiwa wameminywa na lori! Kuna usalama hapo kama siyo neema ya Mungu?” Gari la polisi liliwasili eneo la ajali majira ya saa nane mchana kusaidia uokoaji.

CHANZO: MWANANCHI