KIONGOZI wa upinzani nchini Uganda Kiiza Besigye ameliambia shirika moja la habari Kuwa alitiwa mbaroni na polisi nchini humo mara nne kwa muda wa siku sita kufuatia uchaguzi uliofanyika wiki iliyopita.
Licha ya mshikemshike alioupata matokeo ya uchaguzi huo yalimpa ushindi Rais Yoweri Museven kutawala nchi hiyo kwa muhula wa tano mfululizo. Bw. Besigye ambaye yupo kizuizini nyumbani kwake kwa sasa ameeleza jinsi alivyokamatwa na polisi.
“Nilikamatwa na polisi nikiwa nyumbani mwendo wa saa kumi na moja alfajiri, na kupelekwa kwa mwendo kasi mjini ambao ulikuwa ni mwendo wa kutisha ili kuwakwepa waandishi wa habari waliokuwepo katika eneo walinikamata, na hii ikawa ni mara ya nne kukamatwa na polisi kwa muda wa siku sita.”
Besigye alisema amesikitishwa na kitendo cha jamii ya kimataifa kutoingilia kati suala hilo kwa niaba yake. Aliwaeleza kama fikra zao ni kwamba Rais Museveni ameleta amani na utulivu nchini Uganda wajue wanafanya makosa makubwa.
“Amani na utulivu ni upande mmoja wa sarafu. Upande wa pili wa sarafu ni haki. Hauwezi kuwa na amani na utulivu bila haki. Na hii ndio hali halisi katika mazingira yetu ni kwamba kwa kifupi hakuna haki,” alieleza Besigye katika mahojiano.
-BBC