Na George Binagi-GB Pazzo
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Mwanza imeitupilia mbali kesi ya kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Novemba 25 mwaka jana, katika Jimbo la Tarime Vijijini Mkoani Mara, iliyofunguliwa na aliekuwa mgombea ubunge katika jimbo hilo kupitia Chama cha Mapinduzi CCM Christopher Ryoba Kangoye.
Katika kesi hiyo, wajibu maombi walikuwa ni Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini John Heche (Chadema), Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambapo mtoa maombi alikuwa akiiomba Mahakama kutengua matokeo ya Uchaguzi Mkuu katika Jimbo hilo kwa kuwa haukuwa huru na haki.
Baada ya Mahakama hiyo kupitia kwa Jaji Lameck Mlacha kusikiliza utetezi wa pande zote, iliamua kuifuta kesi hiyo ambayo ilikuwa ni nambari nne ya mwaka 2015 kutokana na hoja
za mleta maombi kuwa na kasoro mbalimbali ikiwemo kutoainisha majina ya waliokuwa wakilalamikiwa kuvuruga uchaguzi Jimboni humo.
Wakili wa mleta maombi Costantine Mutalemwa pamoja na Wakili wa mjibu maombi Paul Kipeja
aliekuwa akisaidiana na Wakili Tundu Lisu katika kesi hiyo, wameelezea kuridhika na maamuzi ya Mahakama hiyo.
Naye Mwl. Chacha Heche ambae ni Katibu wa Chadema mkoani Mara, ameelezea kuwa na imani na Mahakama kutokana na maamuzi iliyoyatoa katika kesi hiyo pamoja na kesi nyingine zilizowahi kuamuliwa Mahakamani hapo na kuongeza kuwa sasa kazi imebaki moja kwa Heche ambayo ni kuwatumikia wakazi wa Jimbo la Tarime Vijijini.
Kwa upande wake Mrimi Zabloni ambae ni Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, ameelezea furaha kwa wananchi wa jimbo hilo huku akiwasihi kuweka imani na Mahakama hapa nchini katika kutoa maamuzi ya kesi mbalimbali.
Wananchi wengi Mahakamani hapo kutoka Jimboni Tarime Vijijini walikuwa ni wafuasi wa Chadema na wameonyesha kuyapokea maamuzi ya mahakama hiyo kwa furaha kubwa na kwamba wao waliamua ushindi wa Heche tangu Novemba 25 mwaka jana kwenye daftari la kupigia kura.
Kesi hiyo ilisikilizwa Januari 19, 2016 mwaka huu na kuahirishwa hadi juzi Januari 27, 2015 kwa ajili ya kutolewa maamuzi, lakini pia iliahirishwa hadi jana Januari 28, 2016 ambapo maamuzi yameweza kutolewa.