Na Mwanahamisi Matasi – Maelezo
WIRAZA ya Afya na Ustawi wa Jamii imeanzisha kituo cha kuratibu matukio ya sumu nchini kilichopo katika maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Hayo yamesemwa na Mratibu wa Kituo cha Kuratibu Matukio ya Sumu Nchini Bw. Yohana Mshasi alipokuwa anazungumza na Waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam na kutoa Elimu ya matumizi na madhara ambayo yanaweza kutokea kwa jamii kutokana na sumu au kemikali.
“Ili kuweza kupunguza matukio ya matumizi ya sumu ni muhimu kila mwananchi atambue na apatiwe Elimu ya matumizi ya sumu na madhara yake kwa jamii,” alisema Mshasi.
Kituo hicho ambacho kimefunguliwa rasmi Disemba 4 mwaka 2014 kikiwa kina wajibu wa kutoa na kupokea taarifa za matukio ya sumu, kufanya uchunguzi wa kimaabara, kutoa ushauri wa matibabu na kutunza takwimu.
Aidha Mshasi alieleza njia za kuepuka madhara yanayoweza kutokea kutokana na sumu au kemikali na kutoa ushauri kwa Wananchi kuwa wawe wanatoa taarifa pindi yanapotokea matukio ambayo ni hatarishi mfano ajali zinazohusisha kemikali au sumu yoyote, matumizi mabaya ya kemikali kama vile Tindikali, Zebaki, Cyanide na kutoa taarifa pindi wanapoona kuna usafirishaji holela wa kemikali katika mamlaka husika.
Aliendelea kusema kuwa tangu kituo kianzishwe kimekuwa na faida mbalimbali kama vile kuokoa maisha ya watu wanaoumwa na kupunguza idadi ya vifo, kuiwezesha jamii kuepuka gharama ambazo wangezitumia kwa matibabu, na pia kuokoa muda au wakati kwa kutambua madhara madogo madogo ya sumu ambayo yanaweza kupatiwa suluhisho majumbani kwa ushauri wa huduma ya kwanza kutoka katika kituo.
Kwa mujibu wa takwimu nchi ya Uholanzi ndio nchi ya kwanza iliyoanza kutoa huduma hii na kufuatiwa na Marekani na baadae kuenea Afrika na kwa Tanzania kituo kilifunguliwa na kuwa chini ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Ili kutimiza lengo la afya kwa wote, shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) walitoa mwito wa kujenga vituo vya kuratibu matukio ya sumu katika sehemu zenye uwezo wa kuchunguza na kutambua sumu ili tiba sahihi iweze kutolewa na Wizara ya Afya ikatenga kituo cha maabara cha kuratibu wa matukio ya sumu chini ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kujengewa uwezo ili kutimiza malengo.