Na Mwandishi Wetu
KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen leo ametangaza kikosi cha wachezaji 22 kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Chad itakayochezwa Novemba 11 mwaka huu jijini N’Djamena.
Poulsen ametangaza kikosi hicho leo alipozungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam. Mchezaji aliyeitwa kwa mara ya kwanza ni kipa Mwandini Ally wa Azam huku pia akimjumuisha kwenye kikosi chake mshambuliaji wa timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes), Thomas Ulimwengu.
Akitaja kikosi hicho, amebainisha magolikipa ni Juma Kaseja (Simba) na Mwadini Ally (Azam). Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Juma Nyoso (Simba), Idrissa Rajab (Sofapaka, Kenya), Erasto Nyoni (Azam), Nadir Haroub (Yanga), Godfrey Taita (Yanga) na Juma Jabu (Simba).
Viungo ni Henry Joseph (Kongsvinger IL, Norway), Nurdin Bakari (Yanga), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Abdi Kassim (DT Long An, Vietnam), Ramadhan Chombo (Azam) na Shomari Kapombe (Simba).
“Washambuliaji katika kikosi hicho ni Nizar Khalfan (Vancouver Whitecaps, Canada), Mrisho Ngassa (Azam), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Dan Mrwanda (DT Long An, Vietnam), Athuman Machupa (Vasalund IF, Sweden), Hussein Javu (Mtibwa Sugar) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC),” amesema Poulsen.
Amesema timu itaingia kambini Novemba 3 mwaka huu jijini Dar es Salaam, na inatarajiwa kuondoka nchini Novemba 9 mwaka huu kwenda N’Djamena kwa ajili ya mechi hiyo. Stars na Chad zitarudiana Novemba 15 mwaka huu jijini Dar es Salaam.