MABINGWA watetezi Uhispania wamefuzu kuingia fainali ya Euro 2012, baada ya kuishinda Ureno magoli 4-2, kupitia mikwaju ya penalti, baada ya muda wa kawaida wa dakika 90 na dakika 30 za ziaida kumalizika kwa timu hizo mbili kushindwa kufungana.
Bao la mwisho la mikwaju ya penalti kwa Uhispania lilitiwa wavuni na Cesc Fabregas, na kuwapa wenzake matumaini ya kutetea ubingwa wao kikamilifu, watakapocheza aidha na Ujerumani au Italia katika fainali ya Jumapili.
Fabregas, ambaye ni kiungo cha kati wa timu ya Barcelona, alipiga mkwaju ambao baada ya kugonga mwamba upande wa kushoto, ulitambaa wavuni, na ikawa ni tiketi ya Uhispania kufanya mipango ya kusafiri hadi Kiev, Ukraine, kwa fainali.
Mchezaji wa Ureno, Bruno Alves, alielekea kuwa na wasiwasi, na kushindwa kufunga mkwaju wake, baada ya mpira kugonga mwamba, na Ronaldo, akiwa amepangwa na timu yake katika nafasi ya tano kwa wapigaji penalti, hakupata hata nafasi ya kutimiza wajibu huo.
Wengine waliokosa kufunga kupitia mikwaju ya penalti ni mchezaji wa Ureno, Joao Moutinho, wakati kipa wa Uhispania, Casillas, alipoweza kuokoa kwa kuruka upande wa kkulia.
Awali mchezaji wa Uhsipania Xabi Alonso naye alikosa kutumbukiza wavuni mkwaju wa penalti, licha ya kwamba ulikuwa ni mkwaju wa kasi na uliopigwa kwa nguvu, lakini kipa Rui Patricio akauzuia.