WATU 16, wakiwemo wanaume 11 na wanawake 5, wamekatwa na Jeshi la Polisi kufuatia vurugu za kugombea malisho katika Kijiji cha Miti Mirefu, wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, baina ya jamii ya kifugaji ya Ki-maasai na Mwekezaji wa shamba la ndarakwai Peter Jones, ambapo magari tisa yaliteketezwa kwa moto huku nyumba zaidi ya 16 zikichomwa moto.
Akidhibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama, amesema kuwa watu hao ambao ni jamii ya kifugaji, walikamatwa jana kufuatia operesheni kubwa iliyofanywa na jeshi hilo.
Gama ambae pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Kilimanjaro, amesema vifaa hivyo vilivyokamatwa ni pamoja na kompyuta mpakato, magodoro, vitanda, meza na vitu vingine vya dhamani.
Akielezea zaidi sakata la mgogoro huo, Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa Novemba, 19, kamati za ulinzi na usalama za wilaya za Longido, mkoani Arusha na ile ya wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, zitakutana ili kutoa tamko kuhusiana na eneo la mgogoro.
Mwishoni mwa wiki iliyopita watu wanaodaiwa kuwa jamii ya kifugaji walilivamia shamba la mwekezaji huyo, ambaye pia anafanya utalii wa picha, kambi za watalii na kufuga wanyama kama Tembo, Twiga, Pofu na Nyani, na kusbabisha kuwepo kwa vurugu hizo ambazo zilizuka baada ya mifugo zaidi ya 300 ya jamii ya wafugaji wa Ki-maasai kutoka wilaya ya Longido na nchi jirani ya Kenya, walidaiwa kuingiza mifugo yao kwenye shamba la mwekezaji huyo baada ya kukosa eneo la malisho ya mifugo yao.