*Kanyenye arejeshewa ulaji FIFA
MCHAKATO wa kumpata Ofisa wa Ligi bado unaendelea. Kamati ya Ligi ilipitia maombi ya watu 16 yaliyowasilishwa TFF kwa nafasi ya Ofisa huyo kwa ajili ya Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza. Mwisho wa kutuma maombi ilikuwa Desemba 28 mwaka jana.
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura amesema maombi yote 16 yalipitiwa ambapo waliopita katika mchujo huo wa kwanza wataitwa kwa ajili ya usaili. Waombaji wataarifiwa siku ya usaili kupitia mawasiliano waliyotumia wakati wanawasilisha maombi yao.
Amesema katika hatua nyingine, Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limemthibitisha tena mwamuzi msaidizi John Kanyenye wa Tanzania kuingia katika orodha yake kwa mwaka 2012.
Awali FIFA ilituma TFF majina ya jumla ya waamuzi 14 wa Tanzania wakiwemo waamuzi wasaidizi wawili wapya kwa ajili ya mwaka 2012. Jina la Kanyenye halikuwamo katika orodha hiyo iliyokuwa imetumwa awali.
“Kwa vile Kanyenye alikuwamo katika orodha ya waamuzi wa Tanzania wanaotambuliwa na Shirikisho hilo kwa mwaka 2011 na jina lake halikurudi, TFF ililazimika kuiandikia FIFA ili kupata ufafanuzi wa kuenguliwa kwa Kanyenye,” alisema Wambura.
Uamuzi wa FIFA kumrejesha Kanyenye kwenye orodha inaifanya Tanzania sasa kuwa na jumla ya waamuzi 15. Waamuzi wa kati ni Israel Mujuni, Judith Gamba, Orden Mbaga, Ramadhan Ibada na Sheha Waziri. Waamuzi wasaidizi ni Ali Kinduli, Erasmo Clemence, Ferdinand Chacha, Hamisi Chang’walu, John Kanyenye, Josephat Bulali, Khamis Maswa, Mwanahija Makame, Saada Tibabimale na Samuel Mpenzu.