Na Joachim Mushi
Kagera
MENEJA Mkuu wa Kiwanda cha Sukari cha Kagera, Ashwin Rana amesema hakuna upungufu wowote wa bidhaa hiyo nchini, kwani kiwanda hicho pamoja na kile cha Mtibwa kina akiba ya kutosha kusambaza nchini.
Amesema Kiwanda cha Sukari cha Kagera na kile cha Mtibwa (Mtibwa Sugar) ambavyo vyte ni vya mmiliki mmoja vina akiba ya bidhaa hiyo iliyoko stoo ya kutosha kukabiliana na mahitaji ya nchini pamoja na wajeja wake wengine.
Rana alitoa taarifa hiyo juzi mjini hapa alipokuwa akitoa ufafanuzi mbele ya Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), walipofanya ziara kukitembelea kiwanda cha Sukari cha Kagera kuona uzalishaji wake.
Kauli hiyo imekuja wakati idadi kubwa ya Watanzania wakiamini nchi ina upungufu wa bidhaa hiyo kutokana na kupanda bei mara dufu maeneo mbalimbali ya nchi, na tayari Serikali imekusudia kuagiza bidhaa hiyo kutoka nje.
Alisema kiwanda hicho kilichoanza kazi baada ya kubinafsishwa mwaka 2001 kimefanyiwa ukarabati mkubwa wa miundombinu, mitambo anuai ya kiwanda, ununuzi wa nyenzo za kisasa na upanuzi kwa baadhi ya maeneo umekiwezesha kuzalisha tani 120 za sukari kwa saa tangu mwaka 2010.
“Sukari ipo ya kutosha kwenye godauni zetu zote mbili…hadi ninavyoongea hivi tuna takribani tani 5500 za sukari zimekaa, hakuna tatizo lolote, zinasubiri wanunuzi,” alisema Rana akiwaeleza wajumbe wa NSSF waliotembelea kiwanda hicho.
Aliongeza kuwa shehena hiyo kubwa ya sukari ipo pia katika kiwanda cha Mtibwa ambacho kipo chini ya mmiliki mmoja pamoja na cha Kagera. Alisema kulingana na hali ya uzalishaji upungufu wa bidhaa hiyo huenda ukajitokeza kuanzia mwezi Mei.
Akitoa ufafanuzi zaidi kwa wajumbe, Rana alisema awamu ya pili ya ukarabati wa kiwanda inayotarajia kukamilika Juni, 2012 itakiongezea ufanisi kiwanda hivyo kuwa na uwezo wa kuzalisha tani 200 za sukari kwa saa tofauti na ilivyo sasa.
Hata hivyo alibainisha kuwa lengo la kiwanda ni kuhakikisha kinakuwa na uwezo wa kukamua tani 100,000 moja kwa saa ifikapo mwaka 2013, hali ambayo itaongeza ufanisi kwa kiasi kikubwa tofauti na ilivyo sasa.
Awali akitoa taarifa fupi kwa wajumbe hao wa bodi ya NSSF kabla ya kutembelea mitambo na mashamba ya kiwanda, Rana alibainisha kuwa lengo la kiwanda ni kufanya uzalishaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa itakayoongeza uzalishaji kwa kiasi kikubwa.
Alisema jumla ya hekari 1,500 za mashamba mapya ya kiwanda yanaendelea kuandaliwa katika hatua mbalimbali tena kwa teknolojia ya kisasa na tayari kiwanda kimepanda hekari 1150 za zao la miwa kama mali ghafi ya kiwanda.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya NSSF, Abubakar Rajab akitoa shukrani kwa niaaba ya bodi ya shirika baada ya ziara hiyo, alisema bodi imeridhika na kazi nzuri inayofanywa na menejimenti ya kiwanda ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa kisasa.
“Tumetembelea tumeona kazi nzuri inayofanyika hapa, kuna haja ya wakulima na wawekezaji wengine kuja kujifunza hapa kilimo cha umwagiliaji, ni mradi mkubwa na mnaendesha kisasa…hiki ndio Kilimo Kwanza kweli kweli,” alisema. NSSF imekifadhili kimkopo kiwanda cha Sukari Kagera kiasi cha sh. bilioni 12.
Mwisho