‘Acheni kusambaza Ukimwi’

Na Mwandishi Wetu, Makete

WATUMISHI wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete ambao wanajijua wameambukizwa Ukimwi wameshauriwa kuacha kusambaza ugonjwa huo kwa wengine.

Sambamba na mwito huo, wamehimizwa kujitokeza kupima virusi vya Ukimwi kwa hiari mara kwa mara ili kujitambua na kuchukua uamuzi. Ushauri huo umetolewa mjini hapa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Imelda Ishuza wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo yaliyolenga kuweka mikakati ya kupunguza maambukizi ya Vurusi Vya Ukimwi (VVU) kazini.

Alisema watumishi ni nguzo ya kuharakisha maendeleo, hivyo ni vyema kujiepusha na njia hatarishi zinazoweza kuchochea maambukizi ya Ukimwi na magonjwa mengine ya zinaa.

“Kufariki kwa mtumishi hata mmoja katika halmashauri yetu tayari ni pigo kubwa na hadi tupate mfanyakazi mwingine, bado itachukuwa muda mrefu maana itatakiwa apewe mafunzo ili awe kama yule aliyefariki jambo ambalo linahitaji gharama kubwa, jamani tujihadhari” alisisitiza Ishuza.

“Mimi nawaomba ndugu watumishi wenzangu hebu tumieni muda huu ipasavyo kuibuka na mikakati ya kina kupambana na maambukizi mapya ya VVU mahali pa kazi kwani wilaya yetu ni miongoni mwa wilaya zilizokumbwa na tatizo la Ukimwi kwa kiasi kikubwa” aliongeza Ishuza.

Akiwasilisha mada yake katika mafunzo hayo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Makete, Dk. Joseph Gasper alisema jitihada za kupunguza maambukizi katika wilaya hiyo zinaonekana kuzaa matunda, kwani idadi ya maambukizi kwa siku inaonekana kupungua.

Dk. Gasper alizitaja sababu zinazochangia ongezeko la maambukizi ya Ukimwi wilayani Makete kuwa ni pamoja na kufanya ngono nzembe na wajane au wagane kuolewa bila kupima, mwingiliano wa watu wageni, kukaa mbali na wenzi kwa muda mrefu, wanaume kutofanyiwa tohara (kudondosha mkono sweta) wanandoa kutengana na kushirikiana vitu vyenye ncha kali.

Akifunga mafunzo hayo, Ofisa Maendeleo ya Jamii (DCDO), Focus Mwita aliwasihi watumishi kufuata mikakati waliyojiwekea kupambana na maambukizi ya Ukimwi, ikizingatiwa kuwa Makete imepoteza watumishi wake kwa ugonjwa wa Ukimwi.